MAMBO KUMI YA KUZINGATIA ILI KUENDESHA NCHI VIZURI.
Kupitia kazi za Cicero, tunapata mambo kumi ambayo anashauri viongozi wazingatie ili kuendesha nchi zao vizuri.
Kabla hujasema wewe siyo kiongozi wa nchi, nikuambie tu, wewe ni
kiongozi wako binafsi, ni kiongozi wa familia yako, ni kiongozi wa
biashara zako na pia ni kiongozi kwenye eneo lako la kazi. Hivyo mambo
haya kumi yatakusaidia sana kwenye maisha yako, hata kama siyo kiongozi
wa nchi.
Karibu tujifunze mambo haya kumi na jinsi ya kuyatumia kwenye maisha
yetu ili tuweze kuwa na maisha bora na mahusiano mazuri na wengine pia.
(1). Fuata sheria za asili.
Cicero anatuambia zipo sheria za asili ambazo zinaongoza maisha ya
kila kiumbe hapa duniani. Kiongozi yeyote anayetaka kuongoza vizuri,
lazima aweze kufuata sheria hizo za asili.
Sehemu ya sheria hizo za asili ni kwamba watu wote ni sawa, kila mtu
anastahili kupata haki, kila mtu ana uhuru wa kuishi na kufanya maamuzi
yake, na pia kila mtu anayo haki ya kuwa na furaha kwenye maisha yake.
Kama kiongozi, lazima uhakikishe watu wako wana uhuru huo wa maisha, tofauti na hapo uongozi utakuwa mgumu.
(2).Kuwa na mgawanyo wa madaraka.
Kila serikali inapaswa kuwa na mgawanyo wa madaraka, na pia kiongozi
kuwa na njia ya kuhojiwa na kudhibitiwa asije kugeuka na kuwa kiongozi
mbaya.
Cicero aliona jinsi ambavyo viongozi wengi wanaanza na nia nzuri, na
watu wanawaamini sana, wanaacha kuwahoji na kuwadhibiti, na kinachotokea
viongozi au wanabadilika na kuwa madikteta na watawala wabaya sana.
Lazima iwepo njia ya kukufanya wewe kama kiongozi uweze kuhijiwa na
kudhibitiwa, ili kuepuka madhaifu yako ya kibinadamu kuharibu uongozi
wako,
(3). Kuwa na tabia njema na uadilifu wa hali ya juu sana.
Cicero anatuambia kitu pekee kitakachomwezesha kiongozi kuwa bora ni
tabia njema, na kitakachomwezesha kuendelea kuwa kiongozi bora ni
uadilifu wa hali ya juu sana.
Anatuambia kama kiongozi, maslahi ya nchi yako yanapaswa kuwa juu ya
maslahi binafsi. Pale kiongozi anapoanza kujali maslahi yake kwanza,
ndipo ufisadi unapoanzia na uongozi kuwa mbaya sana.
Cicero anasema kama kiongozi, hupaswi hata kutiliwa shaka juu ya
tabia zako au uadilifu wako. Watu watakuamini zaidi pale unapokuwa na
tabia njema na uadilifu wa hali ya juu.
(4). Waweke marafiki karibu, na maadui karibu zaidi.
Cicero anatuambia moja ya udhaifu wa kiuongozi ni watu kuwachukulia
poa marafiki zao, na kuwapuuza maadui wao. Unahitaji kuwaangalia kwa
karibu sana marafiki zako, maana hao ndiyo wanaoweza kuwa wabaya sana
kwa uongozi wako, hasa pale wanapokosa walichotegemea.
Pia anatuambia tuwe makini na maadui zetu, tujue kila wanachofanya ili lisitokee lolote la kutushangaza.
Cicero anasisitiza pia umuhimu wa kushirikiana na wale ambao
wanapingana na uongozi wetu, kwa sababu kupitia wao tunajifunza njia za
kuwa bora zaidi.
(5). Akili na ujuzi
Cicero anasema wale wanaoongoza, wanapaswa kuwa na akili sana.
Anasema lazima kiongozi awe mjuzi wa mambo, na kadiri kiongozi
anavyojua, ndivyo watu wanamwamini na kumheshimu.
Cicero anasema kiongozi asiyekuwa na ujuzi wa kutosha kwenye chochote
anachoongelea, hotuba zao zinakuwa za maneno matupu na matendo yao
yanakuwa hatari sana.
(6).Maelewano ni njia ya kuweza kufikia muafaka.
Cicero anasema kwenye uongozi, kuna wakati utahitaji kukubaliana na
yale usiyokubaliana nayo ili tu kufikia muafaka. Anasema kama kiongozi
hupaswi kuwa na misimamo isiyoyumba, kwa kufanya hivyo utasababisha
matatizo hata kwenye mambo madogo.
Cicero anasema kama kiongozi usibadili maono yako, bali badili njia
ya kufika pale. Hivyo kama ipo njia ya kufika pale, ambayo ni sahihi
lakini ulijiambia hutaipita, na ndiyo njia pekee iliyopo kwa wakati huo,
weka pembeni majigambo yako na fanya kile kinachopaswa kufanywa.
Kama kiongozi kuna wakati utajikuta unalazimika kufanya vitu ambavyo
ulijiahidi hutafanya kabisa. Lakini uongozi una changamoto, lazima
nyakati nyingine ulegeze msimamo ili mambo yaweze kwenda.
(7).Usiongeze kodi, labda kama ni lazima sana.
Cicero anasema hakuna kitu kinawachosha wananchi kama kodi. Na
serikali nyingi zimekuwa zinapandisha kodi kila mara kwa sababu serikali
zinakuwa kubwa na njia pekee ya serikali kupata fedha ni kukusanya
kodi.
Cicero anashauri kama kiongozi, usipandishe kodi kila wakati, labda kama ni muhimu mno na wananchi wajue hivyo.
Pia Cicero anasema jukumu la serikali ni kuwawezesha wananchi wake
kujipatia mali kadiri wawezavyo kisheria, na fikra za viongozi kwamba
wachache wenye mali wanapaswa kunyang’anywa na kugaiwa wale wasiojiweza
ni fikra inayorudisha maendeleo ya wengi nyuma. Kama wapo watu wanaoweza
kujikusanyia mali kwa njia halali, kazi ya serikali ni kuwahakikishia
mali zao hizo zinakuwa salama, na siyo kuchukua na kuwapa wasiokuwa
nacho.
(8).Uhamiaji unaifanya nchi kuwa imara.
Cicero anasisitiza umuhimu wa nchi kupokea wahamiaji kutoka maeneo
mengine. Wahamiaji wanakuja na ujuzi mpya, uzoefu wa tofauti na hata
utamaduni wa tofauti. Ukiangalia nchi nyingi zilizoendelea, ni zile
zilizoruhusu wahamiaji kuingia. Na hata ndani ya nchi moja, kila eneo,
utakuta wahamiaji kutoka mkoa mwingine wana mafanikio makubwa kuliko
waliozaliwa eneo lile.
(9). Usianzishe vita isiyo na umuhimu.
Cicero anasema zipo sababu mbili pekee za nchi kuingia kwenye vita;
Moja ni kujitetea pale nchi inapokuwa imevamiwa, lazima nchi ipigane kuondoa uvamizi.
Mbili ni kulinda heshima ya nchi, pale ambapo nchi inakuwa inachezewa
na watu wengine, inaweza kuingia kwenye vita kulinda heshima yake.
Sababu nyingine yoyote ya nchi kuingia kwenye vita siyo sahihi na italeta madhara kwenye uongozi na nchi kwa ujumla.
(10). Rushwa inaangamiza taifa.
Cicero anasema taifa lolote linaloanguka, anguko huwa linaanzia ndani
na siyo nje. Na anguko linaanzia ndani pale viongozi wanapokuwa na
tamaa, rushwa na udanganyifu. Anasema vitu hivyo vikishakuwa ndani ya
serikali, inakuwa dhaifu kwa nje na rahisi kuangamia.
Kama kiongozi unapaswa kuhakikisha uongozi unakuwa wa uaminifu na
uadilifu wa hali ya juu, na rushwa, tamaa, udanganyifu havipo kabisa
katika uongozi. Wananchi wanakuwa na imani pale wanapogundua viongozi
wao ni wasafi na waadilifu.
Rafiki, hayo ndiyo mambo kumi ya kuzingatia kwenye uongozi wowote
unaoubeba, iwe ni wako binafsi, wa familia, wa kazi, wa biashara na hata
wa nchi. Fanyia kazi mambo hayo kumi ili kuwa kiongozi bora kabisa na
kufikia maono yako makubwa.
Na Mwl Japhet Masatu , Dar es salaam , Tanzania, East Afrika
+255 716 924136 ( WhatsApp ) , + 255 755400128
Email: japhetmasatu@gmail.com
LEADERS & THE WORLD BLOG
AN ONLINE PLATFORM FOR AFRICAN & WORLD LEADERS . ------ ''BE WILLING TO MAKE DECISIONS. '' THAT"S THE MOST IMPORTANT QUALITY IN A GOOD LEADER. ---- GEORGE S. PATTON
Monday, September 24, 2018
Thursday, February 15, 2018
Wednesday, July 26, 2017
Saturday, May 6, 2017
Thursday, May 4, 2017
Subscribe to:
Posts (Atom)