Fukuto
la wapinzani lapania kumwondoa Rais Mugabe
Wed 31 August , 2016
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
NA BALINAGWE MWAMBUNGU,
NILIWAHI kuandika huko nyuma kwamba
viongozi kama Mugabe waogopwe, nikashambuliwa na baadhi ya wasomaji,
hawakujitaja majina, lakini nadhani ni watu waliowahi kuwa karibu na Rais
Robert Mugabe wa Zimbabwe. Nikaambiwa kuwa nilikuwa ‘kasuku’ wa mawazo ya
Kizungu (Eurocentric copy-cat).
Lakini niliyoyaandika miaka 2007
(miaka 9) iliyopita sasa yanatokea nchini Zimbabwe. Maelfu kwa maelfu ya
wananchi wiki iliyopita, waliandamana kupinga utawala wa Mugabe na wakionesha
kuchoshwa na maisha duni yanayotokana na kuanguka kwa uchumi mnamo mwaka 2009,
ufisadi na umasikini unaozidi kuongezeka nchini humo.
Nchi hiyo sasa inatumia fedha aina
mbili Dola ya Zimbabwe (haina thamani) na Dola ya Kimarekani. Aidha, wananchi
wanapinga mipango ya Benki Kuu ya kutaka kubadili noti na kuingiza sokoni dola
mpya kwamba itakuwa na madhara makubwa na watu wengi waliojiwekea akiba,
watafilisika.
Wakati naandika wakati ule, Zimbabwe
ilikuwa imetoka kufanya Uchaguzi Mkuu na nilivinukuu vyombo vya nje na
waangalizi wa kimataifa waliotamka bayana uchaguzi ule haukuwa huru na wa haki.
Wananchi wa Zimbabwe (kama
Watanzania katika Uchaguzi Mkuu uliopita), walishindwa kufanya mabadiliko ya
kisiasa, japo dalili zote zilionekana kwamba upinzani ulikuwa na nguvu na uwezo
wa kukiondoa madarakani chama cha Rais Mugabe cha ZANU-PF.
Rais Mugabe (92), amekuwa madarakani
kwa miaka 36 sasa. Amekuwa akiendesha chaguzi kama kiini macho tu kama
wafanyavyo baadhi ya viongozi barani Afrika. Ni nchi chache sana ambazo
zimewahi kuendesha chaguzi huru na za haki katika Afrika.
Viongozi wengi walio madarakani,
hawataki kuondoka na hivyo kutumia hila nyingi ili waonekane bado wanakubalika
na wananchi.
Nguvu za kisiasa za Mugabe
zilitokana na kuungwa mkono na wanajeshi waliopigana kwenye vita vya msituni
vilivyoangusha utawala wa Wazungu wachache walowezi na Waafrika vibaraka.
Lakini kabla ya maandamano ya Ijumaa iliyopita, Maveterani wa vita vya msituni
nao maji yamewafika shingoni.
Hali yao ya maisha ni mbaya. Mapema mwezi
huu, waliandamana na kwa mara ya kwanza wakasusia hotuba ya Rais Mugabe katika
sherehe za kila mwaka za kuwaenzi. Maveterani hao walimtaka Mugabe aachie ngazi
na baadhi yao walikamatwa na polisi. Maveterani pia wanadai nyongeza ya
pensheni. Badala ya kukaa kitako na kuwasikiliza, Serikali ya Mugabe ikawapiga
kwa mabomu ya moshi na kuwatawanya.
Sasa Maveterani hao kupitia chama
chao cha Zimbabwe National Liberation War Veterans, wameamua kumuunga mkono
aliyekuwa Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Joyce Mujuru, ambaye wanasema alikuwa na
mchango mkubwa wakati wa vita ya ukombozi. Mujuru aliunda chama chake cha
Zimbabwe People First (ZPF), baada ya kufukuzwa kazi na Mugabe.
Katibu Mkuu wa Chama cha Maveterani,
Victor Matemadanda, alinukuliwa akisema kwamba Mujuru alitumikia Zimbabwe
katika nafasi mbalimbali kama waziri kwa miaka 34 na hakuna kiongozi yeyote wa
ZANU-PF aliyewahi kumnyooshea kidole kwamba alikuwa na mapungufu, lakini baada
ya kuondoka, wanampiga madongo.
Anaanika kwamba vigogo wengi ndani
ya ZANU-PF si wasafi katika mambo yao binafsi. “Kumpiga madongo Mujuru ni sawa
na kuliambia taifa kwamba katika ZANU-PF hakuna kiongozi aliye msafi kwa kuwa
ukiwa ndani ya chama hakuna atakayesema mabaya yako, lakini ukitoka na
unakikosoa chama, unakuwa adui,” alikaririwa Matemadanda.
Wakati wa uchaguzi, ZANU-PF
kinatumia vyombo vya ulinzi na usalama kuhujumu haki ya raia ya kubadilisha
uongozi kwa njia ya sanduku la kura. Wanasaidia kuhujumu demokrasia. Wanawaliza
wapinzani kwa kuiba kura kwa njia ya elektroniki wakati wa majumuisho
(tallying).
Mchezo hufanyika nyuma ya Tume ya
Uchaguzi na waangalizi ambao wanakuwa hawajui kinachoendelea nyuma ya pazia.
Mtindo wa zamani wa kuwajaza kura za wizi kwenye masanduku ya kura au kuyaondoa
baadhi ya majina kwenye orodha ya wapiga kura hasa katika maeneo ambako walijua
kuwa ni ngome ya upinzani, umepitwa na wakati.
Lakini labda si ZANU-PF tu ya Mugabe
ni mchezo mchafu ambao unahujumu matakwa ya wananchi ya kufanya mabadiliko.
Mchezo huu pia hudumaza demokrasia na kukatisha wananchi tamaa.
Mugabe na umri wake mkubwa, anajiona
kuwa ni ‘jongwe’, jogoo pekee katika Zimbabwe akidhani kwamba bila yeye hakuna
Zimbabwe. Wako viongozi katika chama tawala hapa nchini ambao kama Mugabe,
wanadhani bila Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchi itakwama. Wanasahau kabisa kwamba
wao wataondoka, Tanzania itabaki.
Mugabe amesema atagombea tena katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2018 na anajitapa kwamba yeye ‘ni Mungu’. Anasahau
kwamba Mungu ndiye yote katika yote. Na vivyo hivyo kuna baadhi ya viongozi
hapa Tanzania, wanatamka wazi kwamba chama chao kitatawala kwa miaka mingine
100, ila wanasahau kwamba dunia inabadilika na kwamba wao hawatakuwapo wakati
huo.
Mugabe amepangua pangua uongozi
ndani ya ZANU-PF na kuwaweka kando wenye nia ya kumrithi, wengine wakisingiziwa
kutaka kumroga! Sasa inazungumzwa wazi wazi kwamba ama atamwachia madaraka
mkewe Grace au Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa.
Lakini wakosoaji wanasema amejenga
mtandao wa kiukoo ‘Mugabe Dynasty’, ukoo wa watawala kama ilivyo katika nchi za
utawala wa kifalme. Siku moja mwandishi wa habari Mwingereza alimuuliza
lini atastaafu, naye akamrushia swali: Malkia wa Uingereza atastaafu lini?
Baadhi ya wanaharakati, wakiongozwa
na Mchungaji Evan Mawarire, mwanaharakati anayetaka mabadiliko, ndiye aliyewatia
hamasa Wazimbabwe waanze kudai haki zao.
Amejenga fukuto la wananchi
linalojulikana kama ‘This Flag’, linaloongozwa na dhamira ya; Why must we be in
this situation: Kwanini tuendelee kuwa katika hali hii, wanadai maisha bora na
wanataka Mugabe ang’atuke mapema. Lakini yeye anasema muda wake bado na kwamba
hapatakuwa na ‘Arab Spring’ nchini Zimbabwe.
Wachunguzi wa mambo nchini Zimbabwe,
wanasema ikiwa Mugabe ameshindwa kusoma alama za nyakati. Vyama vya upinzani 18
na wanaharakati wameungana na kumwambia ni wakati mwafaka kuondoka madarakani.
Maandamano makubwa yaliyofanyika Ijumaa iliyopita, pamoja na kwamba Mahakama
ilitoa amri kwamba yasiingiliwe, polisi waliwatawanya waandamaji kwa mabomu na
kusababisha vurugu kubwa katika Mji Mkuu wa Harare.
Kiongozi mwandamizi wa chama cha
ZPF, Didymusb Mutasa, alikaririwa akisema Serikali inayojidai kufuata Katiba,
inavunja sheria ilizozitunga yenyewe kwa kuanzisha vurugu na kuanza kuwapiga
wananchi ambao walikuwa wamekusanyika kwa amani. Viongozi wa vyama vya upinzani
wamesema, maandamano hayo yalikuwa ni mwanzo tu. “Tutakuwa mitaani tena Ijumaa
ijayo,” alisikika mmoja wao akisema.
GAZETI LA MTANZANIA