Monday, September 24, 2018

JINSI YA KUENDESHA NCHI ( HOW TO RUN A COUNTRY ) NA MARCUS TULLIUS CICERO

MAMBO KUMI YA KUZINGATIA ILI KUENDESHA NCHI VIZURI.
Kupitia kazi za Cicero, tunapata mambo kumi ambayo anashauri viongozi wazingatie ili kuendesha nchi zao vizuri.
Kabla hujasema wewe siyo kiongozi wa nchi, nikuambie tu, wewe ni kiongozi wako binafsi, ni kiongozi wa familia yako, ni kiongozi wa biashara zako na pia ni kiongozi kwenye eneo lako la kazi. Hivyo mambo haya kumi yatakusaidia sana kwenye maisha yako, hata kama siyo kiongozi wa nchi.
Karibu tujifunze mambo haya kumi na jinsi ya kuyatumia kwenye maisha yetu ili tuweze kuwa na maisha bora na mahusiano mazuri na wengine pia.
(1). Fuata sheria za asili.
Cicero anatuambia zipo sheria za asili ambazo zinaongoza maisha ya kila kiumbe hapa duniani. Kiongozi yeyote anayetaka kuongoza vizuri, lazima aweze kufuata sheria hizo za asili.
Sehemu ya sheria hizo za asili ni kwamba watu wote ni sawa, kila mtu anastahili kupata haki, kila mtu ana uhuru wa kuishi na kufanya maamuzi yake, na pia kila mtu anayo haki ya kuwa na furaha kwenye maisha yake.
Kama kiongozi, lazima uhakikishe watu wako wana uhuru huo wa maisha, tofauti na hapo uongozi utakuwa mgumu.
(2).Kuwa na mgawanyo wa madaraka.
Kila serikali inapaswa kuwa na mgawanyo wa madaraka, na pia kiongozi kuwa na njia ya kuhojiwa na kudhibitiwa asije kugeuka na kuwa kiongozi mbaya.
Cicero aliona jinsi ambavyo viongozi wengi wanaanza na nia nzuri, na watu wanawaamini sana, wanaacha kuwahoji na kuwadhibiti, na kinachotokea viongozi au wanabadilika na kuwa madikteta na watawala wabaya sana.
Lazima iwepo njia ya kukufanya wewe kama kiongozi uweze kuhijiwa na kudhibitiwa, ili kuepuka madhaifu yako ya kibinadamu kuharibu uongozi wako,
(3). Kuwa na tabia njema na uadilifu wa hali ya juu sana.
Cicero anatuambia kitu pekee kitakachomwezesha kiongozi kuwa bora ni tabia njema, na kitakachomwezesha kuendelea kuwa kiongozi bora ni uadilifu wa hali ya juu sana.
Anatuambia kama kiongozi, maslahi ya nchi yako yanapaswa kuwa juu ya maslahi binafsi. Pale kiongozi anapoanza kujali maslahi yake kwanza, ndipo ufisadi unapoanzia na uongozi kuwa mbaya sana.
Cicero anasema kama kiongozi, hupaswi hata kutiliwa shaka juu ya tabia zako au uadilifu wako. Watu watakuamini zaidi pale unapokuwa na tabia njema na uadilifu wa hali ya juu.
(4). Waweke marafiki karibu, na maadui karibu zaidi.
Cicero anatuambia moja ya udhaifu wa kiuongozi ni watu kuwachukulia poa marafiki zao, na kuwapuuza maadui wao. Unahitaji kuwaangalia kwa karibu sana marafiki zako, maana hao ndiyo wanaoweza kuwa wabaya sana kwa uongozi wako, hasa pale wanapokosa walichotegemea.
Pia anatuambia tuwe makini na maadui zetu, tujue kila wanachofanya ili lisitokee lolote la kutushangaza.
Cicero anasisitiza pia umuhimu wa kushirikiana na wale ambao wanapingana na uongozi wetu, kwa sababu kupitia wao tunajifunza njia za kuwa bora zaidi.
(5). Akili na ujuzi
Cicero anasema wale wanaoongoza, wanapaswa kuwa na akili sana. Anasema lazima kiongozi awe mjuzi wa mambo, na kadiri kiongozi anavyojua, ndivyo watu wanamwamini na kumheshimu.
Cicero anasema kiongozi asiyekuwa na ujuzi wa kutosha kwenye chochote anachoongelea, hotuba zao zinakuwa za maneno matupu na matendo yao yanakuwa hatari sana.
(6).Maelewano ni njia ya kuweza kufikia muafaka.
Cicero anasema kwenye uongozi, kuna wakati utahitaji kukubaliana na yale usiyokubaliana nayo ili tu kufikia muafaka. Anasema kama kiongozi hupaswi kuwa na misimamo isiyoyumba, kwa kufanya hivyo utasababisha matatizo hata kwenye mambo madogo.
Cicero anasema kama kiongozi usibadili maono yako, bali badili njia ya kufika pale. Hivyo kama ipo njia ya kufika pale, ambayo ni sahihi lakini ulijiambia hutaipita, na ndiyo njia pekee iliyopo kwa wakati huo, weka pembeni majigambo yako na fanya kile kinachopaswa kufanywa.
Kama kiongozi kuna wakati utajikuta unalazimika kufanya vitu ambavyo ulijiahidi hutafanya kabisa. Lakini uongozi una changamoto, lazima nyakati nyingine ulegeze msimamo ili mambo yaweze kwenda.
(7).Usiongeze kodi, labda kama ni lazima sana.
Cicero anasema hakuna kitu kinawachosha wananchi kama kodi. Na serikali nyingi zimekuwa zinapandisha kodi kila mara kwa sababu serikali zinakuwa kubwa na njia pekee ya serikali kupata fedha ni kukusanya kodi.
Cicero anashauri kama kiongozi, usipandishe kodi kila wakati, labda kama ni muhimu mno na wananchi wajue hivyo.
Pia Cicero anasema jukumu la serikali ni kuwawezesha wananchi wake kujipatia mali kadiri wawezavyo kisheria, na fikra za viongozi kwamba wachache wenye mali wanapaswa kunyang’anywa na kugaiwa wale wasiojiweza ni fikra inayorudisha maendeleo ya wengi nyuma. Kama wapo watu wanaoweza kujikusanyia mali kwa njia halali, kazi ya serikali ni kuwahakikishia mali zao hizo zinakuwa salama, na siyo kuchukua na kuwapa wasiokuwa nacho.
(8).Uhamiaji unaifanya nchi kuwa imara.
Cicero anasisitiza umuhimu wa nchi kupokea wahamiaji kutoka maeneo mengine. Wahamiaji wanakuja na ujuzi mpya, uzoefu wa tofauti na hata utamaduni wa tofauti. Ukiangalia nchi nyingi zilizoendelea, ni zile zilizoruhusu wahamiaji kuingia. Na hata ndani ya nchi moja, kila eneo, utakuta wahamiaji kutoka mkoa mwingine wana mafanikio makubwa kuliko waliozaliwa eneo lile.
(9). Usianzishe vita isiyo na umuhimu.
Cicero anasema zipo sababu mbili pekee za nchi kuingia kwenye vita;
Moja ni kujitetea pale nchi inapokuwa imevamiwa, lazima nchi ipigane kuondoa uvamizi.
Mbili ni kulinda heshima ya nchi, pale ambapo nchi inakuwa inachezewa na watu wengine, inaweza kuingia kwenye vita kulinda heshima yake.
Sababu nyingine yoyote ya nchi kuingia kwenye vita siyo sahihi na italeta madhara kwenye uongozi na nchi kwa ujumla.
(10). Rushwa inaangamiza taifa.
Cicero anasema taifa lolote linaloanguka, anguko huwa linaanzia ndani na siyo nje. Na anguko linaanzia ndani pale viongozi wanapokuwa na tamaa, rushwa na udanganyifu. Anasema vitu hivyo vikishakuwa ndani ya serikali, inakuwa dhaifu kwa nje na rahisi kuangamia.
Kama kiongozi unapaswa kuhakikisha uongozi unakuwa wa uaminifu na uadilifu wa hali ya juu, na rushwa, tamaa, udanganyifu havipo kabisa katika uongozi. Wananchi wanakuwa na imani pale wanapogundua viongozi wao ni wasafi na waadilifu.
Rafiki, hayo ndiyo mambo kumi ya kuzingatia kwenye uongozi wowote unaoubeba, iwe ni wako binafsi, wa familia, wa kazi, wa biashara na hata wa nchi. Fanyia kazi mambo hayo kumi ili kuwa kiongozi bora kabisa na kufikia maono yako makubwa.

Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar es  salaam , Tanzania, East  Afrika
+255 716 924136 ( WhatsApp ) , + 255 755400128
Email: japhetmasatu@gmail.com

No comments:

Post a Comment