Friday, June 10, 2016

JPM APONGEZWA SAKATA WASIO NA SIFA UDOM

 Rais   John   Magufuli

MTANDAO wa Wanafunzi Nchini (TSNP) umemuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuwachukulia hatua za kuwawajibisha waliohusika kuwadahili wanafunzi wasio na sifa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Aidha, mtandao huo umeishauri serikali kusitisha programu maalumu ya kusomesha walimu wa masomo ya sayansi ili kutoa fursa kwa wanafunzi waliodahiliwa kumaliza masomo yao na pia serikali kupanga utaratibu mpya.
TSNP pia imeiomba serikali kuwaruhusu wanafunzi ambao wamebakiza mwaka mmoja wa kumaliza masomo yao ya Stashahada (Diploma) waendelee na masomo yao. Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa mtandao huo, Alphonce Lusako katika mkutano wa kutoa tamko la mtandao huo pamoja na la wanafunzi waliofukuzwa UDOM.
Lusako alisema, hatua hiyo haiepukiki kutokana na wahusika kudahili kinyume na vigezo vilivyowekwa na serikali. Aidha, alisema mtandao huo ulikuwa ukifanya utafiti wa kina kupitia Idara ya Tafiti na Mafunzo ya mtandao huo kuhusu sakata hilo.
Alisema serikali ilianzisha programu hiyo kwa lengo la kutatua uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na kuwekwa sifa za udahili, lakini hatimaye Waziri mwenye mamlaka aliondoa na kuongeza kuwa ikitokea mwanafunzi au kundi la wanafunzi halitapewa haki zao, mtandao huo utashirikiana na wadau wa elimu zikiwemo Asasi za kiraia kufungua kesi mahakamani ili kudai haki zao.
Akisoma taarifa rasmi ya wanafunzi waliosimamishwa UDOM, Gibson Johnson alisema, wanaiomba serikali kuangalia uwezekano wa wao kuendelea na masomo yao.
“Tunaiomba na kuililia serikali iangalie wale wenye division I, II na III ituache tumalizie masomo yetu, lakini watakaokuwa na ufaulu wa chini kuanzia division IV itafute namna ya kuwasaidia,” alisema Johnson.
Wamemuomba Rais Magufuli na Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuona haja ya kuwarudisha chuoni ili kumaliza masomo yao kama ilivyopangwa, kama jambo hilo likishindikana serikali ifanye mkakati wa kuwatafutia vyuo stahiki ili wamalize masomo yao.

CHANZO  CHA  HABARI ,  HABARI  LEO,  Na  Katuma  Masamba , 05  JUNI , 2016.

WAFAHAMU MARAIS 44 WALIOIONGOZA MAREKANI



RAIS Barack Hussein Obama, aliyetembelea Tanzania katika ziara yake ya kiserikali ya siku tatu ni rais wa 44 wa taifa ikimananisha kuwa ametanguliwa na marais wengine 43 tangu taifa hili lilipoasisiwa.  

Orodha ya marais hao kuanzia George Washington, ambaye ndiye rais wa kwanza wa Marekani mpaka huyu wa sasa, Obama, huku miaka waliyoongoza ikiwa kwenye mabano ni kama ifuatavyo:  George Washington (1789-17970)  (2)  John Adams (1797-1801) (3) Thomas Jefferson (1801-1809) (4) James Madison (1809-1817), (5) James Monroe (1817-1825)  (6) John Quincy Adams (1825-1829) (7) Andrew Jackson (1829-1837) (8) Martin Van Buren (1837-1841) (9) William H. Harrison (1841) (10) John Tyler (1841-1845) (11) James K. Polk (1845-1849).

Waliofuata ni:  (12)  Zachary Taylor (1849-1850)  (13) Millard  Fillmore (1850-1853)  (14) Franklin Pierce (1853-1857) (15) James Buchanan  (1857-1861) (16) Abraham Lincoln (1861-1865) (17) Andrew Johnson  (1865-1869) (18)  Ulysses S. Grant (1869-1877) (19) Rutherfold B. Hayes  (1877-1881) (20) James A. Garfield (1881) (21)  Chester A. Arthur (1881- 1885) (22)  Grover Cleveland (1885-1889) (23) Benjamin Harrison  (1889-1893) (24) Grover Cleland (huyu ilikuwa ni mara ya pili kutawala ukiacha kipindi kile alichokuwa rais wa 22) (1893-1897) (25) William McKinley (1897-1901).

Wengine ni: (26) Theodore Roosevelt (1901-1909) (27) William H. Taft (1909 – 1913) (28) Woodrow Wilson (1913-1921)- huyu  alikuwa msomi na Professa wa Chuo Kikuu.

Rais wa  29 alikuwa ni Warren G. Harding  (1921-1923), (30) Calvin Coollidge (1923-1929) (31) Herbert C. Hoover (1929-1933) (32) Franklin D. Roosevelt (1933-1945) (33) Harry S. Truman (1945-1953) (34)  Dwight D. Eisenhower  (1953-1961), (35) John  F. Kennedy (1961- 1963), (36) Lyndon B. Johnson (1963-1969), (37) Richard M. Nixon (1969-1974), (38) Gerald R. Ford (1974-1977).

Wengine ni 39 Jimmy Carter (1977-1981) (40),  Ronald Reagan (1981- 1989), (41) George  H. W.  Bush (1989-1993), (42)  Bill J. Clinton (1993- 2001)  43.  George W. Bush  (2001- 2009) na  44  Barack Hussein Obama (2009-    ).

OBAMA NI NANI  
Obama, ambaye amekuwa kipenzi cha mataifa mengi duniani, ameweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza mweusi kuwa rais katika historia ya Marekani.

Hakuna aliyetarajia kama taifa hilo linaweza kutawaliwa na mtu mweusi tena mwenye asili ya Afrika, lakini mwaka 2009 mambo yalibadilika.
Uteuzi wake katika Chama cha Democratic uliungwa mkono na mamilioni ya watu duniani, ambapo wasanii nyota nchini humo akiwemo Jay Z walijitokeza hadharani kumsaidia.

Obama alizaliwa Agosti 4, 1961. Mama yake ni Mmarekani na baba yake anatajwa kuwa raia wa Kenya, japo kuna taarifa kuwa kiongozi huyo ni Mtanzania na chimbuko lake ni wilaya ya Serengeti.
Amepata kuishi katika Jiji la Jakarta nchini Indonesia hadi mwaka 1971 aliporudi Marekani na kuishi na babu yake huko Hawaii. Alilelewa na kusomeshwa na babu yake.

Kitaalamu Rais Obama ni mwanasheria, ambapo alipata elimu hiyo katika vyuo vya Ociedenta Los Angeles, Columbia na baadaye Chuo Kikuu cha Harvard, ambapo alitunukiwa shahada yake mwaka 1991.
Alipata kufanya kazi za kijamii katika Jiji la Chicago, baadaye alipata kutumika kufundisha sheria katika Chuo Kikuu cha Chicago.

Mwaka 1996-1998 alichaguliwa kuwa Seneta wa Illinos na baadaye mwaka 2002 hadi 2004 alichaguliwa kuwa Seneta wa Bunge la kitaifa.
Safari yake ya kuandika historia mpya nchini Marekani, ilipata msukumo mwezi Februari 2007, aliposimama hadharani na kuelezea nia yake ya kuiwakilisha Democratic katika kuwania urais wan chi hiyo.

Baada ya kutangaza uamuzi huo, alianza harakati kwa kusaidiwa na watu mbalimbali, ambapo ndani ya Democratic alipata upinzani mkubwa katika mchakato wa kura za maoni.

Mpinzani mkubwa wa Obama alikuwa Hillary Clinton, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton. Mnyukano baina ya Hillary na Obama uliibua mambo mbalimbali, lakini hayakumzuia mwafrika huyo kutimiza ndoto zake za kuandika historia mpya katika taifa hilo.

Katika uchaguzi mkuu wa Marekani, Obama alichuana na Seneta John McCain, ambapo alifanikiwa kumwangusha vibaya na kuzidi kuwa kipenzi cha watu duniani.  

CHANZO   CHA    HABARI ,  UHURU  NEWSPAPER  NA   LUKAS  KISASA.