Merkel azindua jumba la Nyerere Addis Ababa
- 11 Oktoba 2016
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
amezindua jumba jipya makao makuu ya Umoja wa Afrika ambalo limepewa jina la
rais mwanzilishi wa taifa la Tanzania, Julius Nyerere.
Jumba hilo ambalo jina lake kamili
ni Jumba la Amani na Usalama la Julius Nyerere limejengwa kwa ufadhili kutoka
Ujerumani.
Litakuwa makao ya idara ya Amani na
Usalama ya AU na litatumiwa pia na maafisa wa kutoa tahadhari ya mapema kuhusu
mizozo barani pamoja na kuratibu juhudi za kulinda amani za AU.
Ujenzi wa jumba hilo, ambalo ukubwa
wake wa sakafu ni mita 13,500 mraba na linaweza kutumiwa na wafanyakazi 360,
uligharimu euro 27 milioni.
Jumba hilo afisi za kufanyia kazi,
vyumba vya mikutano vya kutumiwa na Baraza la Amani na Usalama, chumba cha
kuratibia shughuli, maktaba na vyumba vya shughuli za pembeni.
Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa rais
wa Tanzania hadi 1985, alikuwa mmoja wa viongozi waanzilishi wa Muungano wa
Nchi za Afrika (OAU) ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Alishiriki sana katika jitihada za
kuendeleza bara la Afrika na kusaidia mataifa ambayo hayakuwa yamepata uhuru
kujipatia uhuru wake.
Mwalimu Nyerere alipigania sana
kumalizwa kwa ubabe wa Wazungu katika nchi za Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika
Kusini, na taifa la Kusini Magharibi mwa Afrika/Namibia (sasa Namibia).
BBC SWAHILI
Jumba hilo limegharimu
euro 27 milioni
Bi Merkel amezuru nchi
kadha za Afrika zikiwemo Mali na Niger. Hapa anaonekana na Rais Mahamadou
Issoufou wa Niger.