Friday, October 14, 2016

MFALME WA THAILAND AFARIKI DUNIA AKIWA NA MIAKA 88



Mfalme wa Thailand Bhumibol Adulyadej afariki dunia akiwa na miaka 88
  • 13 Oktoba 2016


Mfalme wa Thailand Bhumibol Adulyadej, mfalme aliyetawala kwa muda mrefu zaidi duniani, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88, kasri kuu nchini humo imetangaza.
Alikuwa ametawala kwa miaka 70.

Mfalme huyo alienziwa sana nchini Thailand na amekuwa akitazamwa kama nguzo kuu ya kuunganisha taifa hilo ambalo limekumbwa na misukosuko mingi ya kisiasa na mapinduzi ya serikali.
Alikuwa amedhoofika sana kiafya miaka ya karibuni na hajakuwa akionekana hadharani sana.
Kifo chake kimetokea huku Thailand ikisalia chini ya utawala wa kijeshi kufuatia mapinduzi yaliyotekelezwa 2014.
Ikulu ilikuwa awali imeonya kwamba hali yake ya afya ilikuwa imedhoofika zaidi Jumapili.

 Raia walikuwa wamekusanyika nje ya hospitali alimolazwa kumtakia heri 

Raia wa Thailand wamekuwa wakivalia mavazi ya rangi ya waridi kumtakia heri.
Mamia walikusanyika nje ya hospitali ambapo alikuwa akitibiwa.
Anayetarajiwa kumrithi Mfalme Bhumibol ni Mwanamfalme Vajiralongkorn, 63, ambaye huwa havutii watu sana kama babake.

Sheria kali kuhusu familia ya kifalme nchini humo huzuia umma kujadili masuala ya urithi hadharani. Ukipatikana na kosa hilo unaweza kufungwa jela muda mrefu.

Ikizingatiwa mchango muhimu aliotekeleza mfalme huyo kuhakikisha uthabiti wa kisiasa nchini Thailand, suala la mrithi wake litakuwa changamoto kuu kwa serikali, anasema mwandishi wa BBC aliyeko Bangkok Jonathan Head.

King Bhumibol, alizaliwa Cambridge katika jimbo la Massachusetts, nchini Marekani.

Alitawazwa mfalme tarehe 9 Juni 1946 baada ya kifo cha kakake Mfalme Ananda Mahidol.
Ingawa mfalme kikatiba nchini humo hana mamlaka makubwa, Mfalme Bhumibol alitazamwa na wengi kama mfalme aliyetawazwa na Mungu.
 

 
 Mfalme Bhumibol Adulyadej aliheshimiwa sana Thailand