Rais Kabila azuru nchini Tanzania
- 3 Oktoba 2016
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya
Congo DRC Joseph Kabila amewasili Dar es Salaam nchini Tanzania kwa ziara ya
siku tatu.
Amepokelewa na viongozi mbalimbali
wa nchi hiyo akiwemo rais John Magufuli, makamu wa Rais Mama Samia Suluhu
Hassan, Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania balozi Augustine Mahiga , Wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi mbalimbali wa Serikali, Mabalozi na
wananchi.
Image caption Rais Joseph Kabila
akiwasili katika katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere nchini Tanzania
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa
wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Rais Joseph Kabila Kabange amepokea
heshima ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa
ajili yake na baadaye kushuhudia burudani ya vikundi vya ngoma.
Siku ya Jumanne tarehe 04 Oktoba,
2016 rais Joseph Kabila Kabange atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais
John Pombe Magufuli, ataweka jiwe la msingi la jengo la mamlaka ya Bandari
Tanzania (TPA) na baadaye kushiriki dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji
wake Rais John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika ziara yake Rais Kabila
anatarajia pia kuzungumzia masuala ya kisiasa nchini mwake ambapo uchaguzi
uliopangwa kufanyika Novemba mwaka huu umesogezwa mbele mpaka mwakani jambo
ambalo limeleta sintofahamu kwa wananchi wa Kongo.
Kabila ataondoka siku ya Jumatano
kurudi Kinshasa.
BBC SWAHILI