MTANDAO wa Wanafunzi Nchini (TSNP) umemuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuwachukulia hatua za kuwawajibisha waliohusika kuwadahili wanafunzi wasio na sifa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Aidha, mtandao huo umeishauri serikali kusitisha programu maalumu ya kusomesha walimu wa masomo ya sayansi ili kutoa fursa kwa wanafunzi waliodahiliwa kumaliza masomo yao na pia serikali kupanga utaratibu mpya.
TSNP pia imeiomba serikali kuwaruhusu wanafunzi ambao wamebakiza mwaka mmoja wa kumaliza masomo yao ya Stashahada (Diploma) waendelee na masomo yao. Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa mtandao huo, Alphonce Lusako katika mkutano wa kutoa tamko la mtandao huo pamoja na la wanafunzi waliofukuzwa UDOM.
Lusako alisema, hatua hiyo haiepukiki kutokana na wahusika kudahili kinyume na vigezo vilivyowekwa na serikali. Aidha, alisema mtandao huo ulikuwa ukifanya utafiti wa kina kupitia Idara ya Tafiti na Mafunzo ya mtandao huo kuhusu sakata hilo.
Alisema serikali ilianzisha programu hiyo kwa lengo la kutatua uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na kuwekwa sifa za udahili, lakini hatimaye Waziri mwenye mamlaka aliondoa na kuongeza kuwa ikitokea mwanafunzi au kundi la wanafunzi halitapewa haki zao, mtandao huo utashirikiana na wadau wa elimu zikiwemo Asasi za kiraia kufungua kesi mahakamani ili kudai haki zao.
Akisoma taarifa rasmi ya wanafunzi waliosimamishwa UDOM, Gibson Johnson alisema, wanaiomba serikali kuangalia uwezekano wa wao kuendelea na masomo yao.
“Tunaiomba na kuililia serikali iangalie wale wenye division I, II na III ituache tumalizie masomo yetu, lakini watakaokuwa na ufaulu wa chini kuanzia division IV itafute namna ya kuwasaidia,” alisema Johnson.
Wamemuomba Rais Magufuli na Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuona haja ya kuwarudisha chuoni ili kumaliza masomo yao kama ilivyopangwa, kama jambo hilo likishindikana serikali ifanye mkakati wa kuwatafutia vyuo stahiki ili wamalize masomo yao.
CHANZO CHA HABARI , HABARI LEO, Na Katuma Masamba , 05 JUNI , 2016.
No comments:
Post a Comment